User avatar
makoba
Topic Author
Posts: 301
Joined: Wed Jul 26, 2017 10:25 am
Location: Dar es salaam
Contact:

WAHENGA WANA MAMBO! NIMEKUTANA NA KITUKO NDANI YA DALADALA

Fri Jul 28, 2017 2:10 pm

[attachment=0]daladala.JPG[/attachment]
KAMA wasemavyo Waswahili, dunia ina mengi… leo nimeamini, si kwa kituko hiki. Kisa si kisa, labda ni kisasi, sijui!

Basi bwana kama kawaida, nimeamka asubuhi kuwahi katika kibarua changu kilekile cha kuchanganya zege ghorofa lipande. Ila usimwambie mtu siri hii kwa sababu ‘wife’ anajua nafanya kazi kitengo maalumu pale ikulu. Wanawake bila uongo hawaendi, nani atakubali kuolewa na mkoroga zege mjini hapa?

Nisipotee katika lengo, tujikite katika mada. Wakati napanda daladala tulikuwa watatu tu, lakini tulipigana vikumbo almanusura kuuvunja mlango wa wenyewe, hivyohivyo kibishi nikafanikiwa kuzama ndani. ‘Mtoto wa mjini hakosi siti’, nikapata moja ya dirishani, kisha taratibu nikaweka nyau chini.

Safari ikaanza, taratibu, taratibu, kama msafara wa wahenga! Dereva anaendesha, abiria wanaendeshwa na konda naye, anakusanya masurufu yake.

Wakati konda anaendelea kukusanya nauli zake, ndipo alipomfikia bwana mmoja barobaro kajaza misuli, kwa jina yu-aitwa Dizasta! Jina lake tu maajabu! Uchuro huu. Ptuuuuuh!

NINI KIKATOKEA?
Jamaa yule akagoma kulipa nauli, japokuwa sura yake hata bila kutumia ‘kaboni fotini’ iliashiria kabisa alikula chumvi nyingi na bila shaka ni mhusika katika kamati ya wahenga.

Konda kuona jamaa hakubali kulipa nauli akafoka, “sijaja kucheza hapa, we bwana nitakupasua!”

Jamaa naye akajibu, “Kausha basi nitakupa shilingi mia mbili, mi mwanafunzi!”

Watu wote tukashangaa, wengine wakacheka hata vicheko vikamkera sana mhenga huyu. Kwa jazba akajizoazoa katika kiti chake, akasimama na kuanza kulalamika kwa hisia,

“Mimi ni mtoto mdogo sana, mnanionea! Mnanionea!” aliendelea kulalamika, “Basi kama hamuamini, ngojeni basi niwavulie muone kama sina ma…” Kabla hajamaliza, konda akadakia,

“Tutajuaje kama umenyoa?”

Wote tukaangua kicheko! Jamaa akakasirika, akakamata mkanda wa suruali yake ili asaule, kuona hivyo, akina mama wa pwani waliojaaliwa busara, hekima na huruma, wakamwahi, wakambembeleza, “Basi baba, basi baba inatosha, usifanye hivyo utajidhalilisha… basi baba, usilie wala usisaule.”

Safari bado inaendelea hapa, namuona kakaa anakunywa soda na biskuti tulizomnunulia ili kumbembeleza, asilie wala asisaule!
Attachments
daladala.JPG
daladala.JPG (280.15 KiB)
WAVUMILIENI! WANAPIGA PICHA ZA UTUPU ILI WAPATE PESA ZA KUNUNULIA NGUO!

Trending Topics