User avatar
makoba
Topic Author
Posts: 301
Joined: Wed Jul 26, 2017 10:25 am
Location: Dar es salaam
Contact:

MREJESHO BAADA YA KUUJARIBU UCHAWI WA ‘CHUMA ULETE’

Tue Aug 08, 2017 2:23 pm


[attachment=0]chuma ulete.JPG[/attachment]

BAADA ya kusikia simulizi mbalimbali kuhusiana na ‘chuma ulete’  kwa muda mrefu, nikaamua nijaribu ili niweze kurahisisha maisha. Nilitamani sana zile hadithi za ‘chuma ulete’ ziwe kweli juu yangu. Ninunue bidhaa kisha fedha zinirudie, zikiwa nyingi zaidi. Nile bila jasho.

Baada ya mawazo hayo, siku chache zilizopita nikaamua kwenda kwa mganga mmoja wilayani Bagamoyo ambaye alisifika kwa kutengeneza utaalamu huo.

Nilifika kwa mganga, nikavua viatu kisha nikaingia ndani. Kama kawaida mganga alinikaribisha kwa mapambio ya ‘kilozi’. Zilipigwa chafya nyingi zilizosindikiza maneno yasioeleweka.

Kabla sijamweleza shida iliyonipeleka pale, mganga akaanza kubashiri: “Kijana una matatizo makubwa, mambo yako hayaendi kuna watu wanakuchezea… umekuja kumtambua anayekufanya ushindwe kupiga hatua… “

Mganga mtaalamu, mlozi aliendelea kuongea mambo mengi ambayo sikuhusiana nayo, nilipoona anazidi kupotea, nikamweleza shida iliyonipeleka: “Mzee nimekuja kwa shida moja tu, nataka unipe uchawi wa chuma ulete, nipate pesa bila jasho.”

Mtaalamu alicheka sana, kabla hajatoa tiba akaniomba niweke shilingi laki mbili ndani ya bakuli kubwa lililokuwa umbali mdogo kutoka usawa wa mapaja yake. Nilitembea na fedha ya kutosha, nikaweka kiwango alichotaka.

Alifurahi alipokiona kitita cha fedha, akatamka maneno ambayo sikuyaelewa, kisha akachukua kitu mfano wa kunde, akakimeza.  Akajitikisa kidogo akakitapika, akachukua kipande cha mti, akanuia maneno fulani, baadaye akatoa kitambaa chekundu kilichokuwa na unga mweupe. Alipomaliza hayo, akachanganya vitu vyote katika kitambaa chekundu, akakifunga vizuri na kukishona kwa sindano ya mkono.

“Chukua dawa yako!” alinikabidhi kwa sauti ya kukoroma, “dawa hii nakupa, ukienda dukani, ukitoa noti ya shilingi elfu kumi, mwenye duka atakurudishia elfu ishirini, ukitoa elfu tano, utarudishiwa elfu kumi, pia baada ya muda, fedha zake zitaanza kuhamia kwako. Nenda kijana.”
Niliagana na mganga nikiwa na furaha ya kutoka kimaisha. Nilifika nyumbani usiku, nikalala nikiwa na shauku ya kuanza mkakati wa utajiri asubuhi.

Asubuhi ilifika, nikaenda dukani nikiwa na noti ya shilingi elfu kumi. Nikanunua vocha ya elfu mbili. Nilitegemea mwenye duka angenirudishia elfu ishirini kama nilivyoelezwa na mganga. Haikuwa hivyo, nilipewa fedha kamili, elfu nane!

Nilijaribu duka jingine bila mafanikio. Hakuna fedha iliyozidi. Nikachoka, nikarudi nyumbani kulala.

Mpaka sasa nimejaribu kununua vitu katika maduka mengi bila kile nilichoahidiwa na mganga kutokea. Na sasa nimeamini kuwa nilitapeliwa na siamini tena kama kuna kitu kinaitwa ‘chuma ulete.’ Huu ni uongo tu! Mjinga mimi, mganga kala laki mbili yangu bure!
Attachments
chuma ulete.JPG
chuma ulete.JPG (538.27 KiB)
WAVUMILIENI! WANAPIGA PICHA ZA UTUPU ILI WAPATE PESA ZA KUNUNULIA NGUO!

Trending Topics